Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia Lebanon, katika hafla ya kumbukumbu ya kifo cha Hujjatul-Islam Sayyid Ibrahim Yusuf Murtadha, iliyofanyika katika Husseiniyya ya Deir Qanun Ra’s al-Ain na kuhudhuriwa na kundi la wanazuoni, wanaharakati wa dini, shakhsia za kisiasa, kijamii na kitamaduni pamoja na wananchi, alisisitiza kuwa: Ushia haujawahi kuwa wa ushabiki bali umekuwa ukiulinda Uislamu, jamii ya Kiislamu na umma wa Kiislamu na madhehebu yake yote. Alibainisha kuwa: Mashia wako pamoja na umma na hawajawahi kamwe kupaza kauli ya kujitenga au kujitenga kisiasa na umma.
Sheikh Al-Khatib mwanzoni mwa hotuba yake alisema: Mwenyezi Mungu awalipe malipo makubwa, na ninamuomba amweke Sayyid marehemu, Hujjatul-Islam Sayyid Ibrahim Murtadha, katika rehema zake pana na amkusanye pamoja na baba na mababu zake watukufu, Ahlul-Bayt wa Unabii (a.s). Pia ninatoa pole na rambirambi zangu kwa familia yake tukufu, Aal Murtadha, na ninamuomba Mwenyezi Mungu awape subira na malipo.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia kisha aliuliza: Wajibu wa dini ni nini? Wajibu wa Swala, Saumu, Zaka, Khums na Jihad ni nini? Ni uelewa huu unaonilazimisha kuswali, kunihamasisha kuamrisha mema na kukataza maovu, na kuniongoza kutambua matatizo ya jamii, hatari za kiutamaduni na za kimaisha, na vitisho vinavyoathiri jukumu la dini katika maisha na uwepo wa jamii ya waumini.
Alisisitiza: Sisi hatuna uhusiano na Uislamu kwa misingi ya ushabiki; sisi si kundi linalounganishwa kwa sababu ya ukoo, madhehebu au ujirani. Majina haya ni muhimu, lakini ushabiki si muhimu. Katika Uislamu hakuna ushabiki. Mtume Mtukufu (s.a.w.w) aliulizwa — huku Salman al-Muhammadi akiwa amekaa karibu naye — je, kuipenda kaumu yako ni ushabiki? Akasema: Hapana; ushabiki ni kuwachukulia waovu wa kaumu yako kuwa bora kuliko wema wa kaumu nyingine.
Sheikh Al-Khatib alisema: Sisi tunahusiana na fikra, mtazamo na maarifa; kinachotuunganisha ni haki, njia iliyonyooka, na wito wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w) na Ahlul-Bayt watoharifu (a.s) pamoja na warithi wao miongoni mwa wanazuoni, akiwemo Sayyid Sharif (r.a).
Aliongeza kuwa: Sisi si kundi la kishabiki na hatuna ushabiki baina yetu, wala hatupingani na makundi mengine kwa sababu tu ya kuitwa Mashia. Ndiyo, tunajivunia kubeba jina la Shia, kwa sababu Ushia si ushabiki bali ni kwa ajili ya haki; Ushia ni kwa ajili ya Ali bin Abi Talib, Amirul-Mu’minin (a.s). Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali; popote alipo Ali, hapo ndipo haki ilipo. Basi ikiwa tuko pamoja na Ali, tuko pamoja na haki.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia aliendelea kusema: Hapa narudia kauli ya Imam Muhammad Mahdi Shamsuddin (r.a): Sisi si dhehebu la kikabila, wala si madhehebu yanayopingana na madhehebu mengine; sisi ni Uislamu — kwa adhama yake, roho yake, na misingi na maadili yake ya kibinadamu ambayo yanatuamrisha kuwatendea mema watu wote — miongoni mwa hayo ni kauli ya Mwenyezi Mungu: “Hakika tumewatukuza wana wa Adam.” Hii ndiyo tamaduni yetu na ya wanazuoni wetu, na ni amana waliyoikabidhi kwa watoto wao katika maisha yao yote.
Sheikh Al-Khatib alisisitiza pia: Ushia kamwe haukuwa wa ushabiki, bali ni mlinzi wa Uislamu, jamii ya Kiislamu na umma wa Kiislamu kwa majina na madhehebu yake yote. Sisi tuko pamoja na umma na hatujawahi kamwe kupaza kauli ya kujitenga au kujitenga kisiasa nao.
Daima tumefanya kama alivyosema Imam Ali bin Abi Talib (a.s): “Nitakuwa katika amani muda wa kuwa mambo ya Waislamu yako salama.” Na kama Imam Hasan (a.s) aliyekubali suluhu kwa ajili ya kuulinda umoja; na kama Imam Husayn (a.s) aliyedumisha njia ya mageuzi kwa damu yake safi huko Karbala na kusema: “Sikutoka kwa kiburi, anasa, dhulma wala uharibifu; nilitoka kwa ajili ya kufanya marekebisho katika umma wa babu yangu.”
Damu ya Imam Husayn (a.s) ilitolewa kwa ajili ya umma na dini ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w).
Alieleza kwamba; kukabiliana na adui “Muisraeli” si suala la kimadhehebu, bali ni wajibu wa kitaifa na Kiislamu. Adui huyu ni adui wa umma wote, si wa kundi fulani tu. Hivyo alitoa wito wa kuwa na uelewa, umoja na kukabiliana na hatari halisi inayoutishia umma wa Kiislamu.
Mwisho, Sheikh Al-Khatib alimkumbuka tena marehemu Hujjatul-Islam Sayyid Ibrahim Murtadha, na akirejelea shakhsia yake ya kielimu, kimaadili na ya kujitolea alisema: Alibaki thabiti katika njia ya elimu na utume wake hadi alipokutana na Mwenyezi Mungu. Alimuomba Mwenyezi Mungu amweke katika Pepo ya milele na amkusanye pamoja na mababu zake watoharifu, Muhammad na Aali Muhammad (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao).
Maoni yako